Utangulizi - Maulid PDF  | Print |

Mosi ni basmala. Pili ni hamduliza kwa Mola muweza kwa neema ziso saza. Tatu ni mbawazi na salamu kwa Mtume mwingi wa miujiza. Nne ni kuomba kuenezwa kwa mbawazi na salamu kwa wote Aalize na wote Swahabaze, na kila aliye ongoka kwa nuru za nyendo zao huku anafata kitabu cha miujiza.

Wabaadu tungo za al-Imam al-Allaama, mhakiki wa ilmu za nje na ndani na Shekhe wa tariqa mwenye kukiriwa na ma-Shekhe wa tariqa wa zama na dahari, Sayyidina Abdul-Wahab bin Ahmad bin Ali ash-Sha’araani, radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie, ni tungo zilizo mashuhuri na zina adhimishwa kwa taadhima kubwa kwenye rubaa za wanachuoni wakuu.

Kitabu chake, al-Miizaani-l-Kubraa, mpaka leo hakikupata mithali yake. Hivyo hivyo basi na kile cha Lawaaqih.

Hichi cha pili, anasema mwanazuoni huyo, kakitunga kwa sababu hii. “nimeona ndugu wengi hupekua kutaka kujua kile kilichopungua kwenye dunia yao. Na sikuona yeyote yule aliye pekuapekua kutaka kuona upungufu uliopo kwenye mambo ya dini yake, isipokuwa wachache tu. Ukanipanda wivu wa imani juu yao na juu ya dini yao. Kwa hivyo nikatunga kitabu hichi kumzindua kila mtu kwa yale yaliyopungua kwenye dini yake...

Tuonavyo sisi, kati ya yale yalopungua ni ile darsa aliyoitoa Ngamia aliyemliza kwikwi Mtume wa Mwenyezi Mungu, swala na salamu za Mwenyezi Mungu zimwalie.

Hadithi hiyo ina umuhimu wake katika mwezi huu aliozaliwa Bwana wa Mitume yote na rehema kuu kwa malimwengu yote, kwetu sote.

Kati ya maswali inayozusha ni kwamba je, Ngamia huyu angelikuwa hai kwenye mwezi huu angelifaya nini? Na tukiliungia swali hilo kwa viumbe wasio kuwa wanadamu waliokutana na mtengwa, swala na salamu za Mwenyezi Mungu zimwalie, kila mmoja akasimama kumtetea kwa uwezo wake, vivyo wangelifanya nini?

Kwenye pango alimokuwamo yeye, swala na salamu za Mwenyezi Mungu zimwalie, na Sayyidina Abubakar, radhi za Mwenyezi Mungu zimwalie, mdomoni alitanda Buibui. “Na hakika nyumba dhaifu mno kuliko zote ni jumba la buibui.” Na Njiwa wakataga kumhami mbora wa viumbe. “Kwani hawaoni ndege walioko juu yao namna wanavyokunjua mbawa zao na tena kuzikunja.” Ahaa! palikuwa na Nyoka. “Na Mwenyezi Mungu ameumba kila kinyama kutokana na maji. Wengine katika hao huenda kwa matumbo yao.” Nyoka hakujiweza, hakujimudu. Na shimoni hakukumweka. Akafanya yote aliyoyaweza, ili mradi atoke aone ule wajihi ambao kila aliyeuona kwa imani aliongoka.

Je, wale wa ulimwengu wa mbawa na wale wenye kutambaa kwa matumbo yao wangelikaa hivi hivi tu tangu mwezi huu wa Rabbil-Awwal unaandama na mwisho unatua?

 
 
 

 

Maulid

RocketTheme Joomla Templates